Tangaza Nasi

Wednesday, 16 April 2014

HESABU YA VIJIJI VITATU VYATEKETEA KILA MWAKA KWA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI

Mkurugenzi wa Evidence for Action, Tanzania, Craig John Ferla
Rais wa UTPC, Kenneth Simbaya

baadhi ya walengwa wa mradi

wanahabari wakifuatilia mada


WANAHABARI 48 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, wamepata mafunzo ya namna ya kuandika habari za afya ya uzazi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika katika ukumbi wa hotel ya Lion, jijini Dar es Salaam kwa uratibu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

Kwa kupitia Kampeni ya Mama Ye!, UTPC inashirikiana na asasi ya Evidence for Action yenye makao yake makuu nchini Uingereza kutekeleza mradi huo.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanahabari kukuza uwajibikaji katika kulinda afya ya mama, mzazi na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na ujauzito.

Mkurugenzi wa Evidence for Action, John Craig Ferla aliwaambia wanahabari walioshiriki mafunzo hayo kwamba takwimu za Shirika la afya Duniani (WHO) linaonesha  wajawazito 8,500 pamoja na watoto wachanga 50,000 hufariki dunia kila mwaka hapa nchini kutokana na matatizo yanatokanayo na ujauzito.

Akizungumzia idadi ya wajawazito wanaofariki kila mwaka alisema taifa linapoteza wastani wa watu wanaoishi katika vijiji vitatu kila mwaka. Kwa wastani kijiji kimoja kina watu kati ya 1,500 na 3,000.

Alisema watu hao wanakufa si kwasababu Mungu amewapenda sana na kuamua kukatisha uhai wao ila ni kwasababau ya kukosekana kwa huduma bora za afya katika maeneo yao.

Mshauri wa mradi huo nchini, Dk Moke Magoma alisema Lengo la Millenia namba tano na nne linataka vifo vya wajawazito na watoto vipungue kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2015.

Alisema maisha ya akina na mama na watoto wanaweza kuokolewa kama kutakuwa na huduma bora za afya kwasababu ushahidi wa kitaalamu unaonesha vifo vingi vitokanavyo na matatizo ya uzazi vinazuilika.

Rais wa UTPC, Kenneth Simbaya alisema katika mafunzo hayo kwamba  wanahabari wana nafasi ya kipekee katika kampeni hiyo.

Alisema wanahaabari ni watetezi wa maslai ya jamii wenye wajibu wa kuhakikisha mikakati inayotengenezwa na kuzinduliwa kwa mbwembwe haiishi kwenye makabati ya viongozi wa wahusika.

“Wanahabari tunaweza kuibua hisia na changamoto na tukasaidia kuhamasisha jamii na serikali zao kufikia  mafanikio ya malengo waliojiwekea,” alisema.

Alisema kwa kupitia UTPC, wanahabari nchini kote wanaweza kufika katika maeneo yenye athari kubwa zaidi za upatikanaji wa huduma (vijijini) na kuhamasisha jamii kuchukua hatua.

Katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto, Simbaya alisema kila mtu anawajibu wa kuchukua hatua.


MAGAZETI YA LEO JUMATANO APRIL 16, 2014 Monday, 14 April 2014

WAHIFADHI WA HIFADHI ZA TAIFA WAPEWA MAFUNZO YA UFUATILIAJI NA TATHMINI 
Mkuu wa Chuo Kikuu Ruaha (Ruco), Dk Cephas Mgimwa

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing'ataki

Meneja wa TANAPA ujirani mwema, Ahamed Mbugi
 
Washiriki katika picha ya pamoja na mgeni rasmi

MRADI wa Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) umeanza kutoa mafunzo ya ufuatiliaji na tathmini kwa wahifadhi wa baadhi ya Hifadhi za Taifa nchini.

SPANEST ni mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF)

Mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku nne katika Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) cha mjini Iringa, yalifunguliwa jana na Mkuu wa chuo hicho, Dk Cephas Mgimwa.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema mafunzo hayo yanahusisha wahifadhi kutoka hifadhi ya Ruaha, Kitulo, Katavi, Mikumi, Sadani, Udzungwa na mapori ya akiba yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania.

Alisema ufuatiliaji na tathmini ya shughuli zinazofanywa ndani na nje ya hifadhi ni suala la msingi katika uhifadhi wa rasilimali za Taifa.

Alisema maeneo yaliyohifadhiwa yamekuwa yanakabiliwa na changamoto mbalimbali za ndani na nje ya mipaka yake jambo linalohitaji uhifadhi shirikishi ili kukabiliana na madhara yake.

“Baadhi ya changamoto kubwa katika maeneo yaliyohifadhiwa na kuharibiwa kwa vyanzo vya maji ambayo ni muhimu kwa viumbe hai ndani ya hifadhi na ujangili wa wanyamapori,” alisema.

Akifungua mafunzo hayo, Dk Mgimwa alisema hifadhi za taifa zina mchango mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi kwa taifa kupitia sekta ya utalii.

Alisema ili sekta hiyo iendelee kuimarika ni lazima kila mtanzania ajione ana wajibu wa kulinda rasilimali zilizohifadhiwa kama anavyolinda na kutunza mifugo yake.

“Tunatakiwa kuendelea kuwaelimisha waranzania ili wafahamu thamani ya rasilimali zilizohifadhiwa na jinsi wanavyoweza kushiriki kuzitunza ili ziendelee kuwepo,” alisema.

Alisema Ruco imefurahishwa na uamuzi wa SPABEST wa kufanyia mafunzo hayo watakayoyatumia kuangalia uwezekano wa kuanzisha kozi za utalii na wanyamapori.

“Jina la chuo chetu la Ruaha linaangaza hifadhi ya Ruaha, ili chuo kionekane kina mchango katika kukuza sekta hii ni muhimu tukawa na kozi hizo,” alisema.

Meneja wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) anayeshughulika na ujirani mwema, Ahamed Mbugi alikiomba chuo hicho kwa kuanzia kianze kutoa kozi fupi katika eneo hilo.

“Mkianza na kozi fupi, mtawavutia vijana wengi wanaozunguka hifadhi zetu katika maeneo haya ya kusini. Hilo likifanikiwa litasaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuwaondoa wale wanaojishughulisha na ujangili,” alisema.

Saturday, 12 April 2014

PROFESA MSOLLA KUWANIA TENA UBUNGE KILOLO, AWACHANA WAPINZANI WAKE

Profesa Msolla katika moja ya mikutano yake Kilolo;hapa alikuwa Lulanzi

Pamoja na mvua kubwa na baridi kali wananchi hawa wa kijiji cha Lulanzi walijitokeza

Hawa ni wa kijiji cha Kilolo

Na hapa ndivyo ilivyokuwa Kitowo
MBUNGE wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla amekanusha uzushi unaoenezwa dhidi yake kwamba hatawania tena kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Kusambazwa kwa taarifa hizo jimboni humo kumemkasirisha mbunge huyo ambaye kwa mara nyingine tena, leo hii amewapa matumaini wapiga kura wake kwa kutangaza kuwania kiti hicho katika uchaguzi huo wa mwakani.

Alitangaza azma yake hiyo katika mikutano ya kuhamasisha maendeleo aliyofanya katika vijiji vya Lulanzi, Kilolo na Kitowo.  

“Nitagombea, naomba Mungu anipe afya njema; nitafanya hivyo kwa kuwa nataka mambo yote ya maendeleo niliyoanzisha yafike mahali pake,” alisema huku akishangiliwa na wananchi wa vijiji hivyo.

Alisema CCM ni chama kinachoamini katika demokrasia ya kweli na ya uwazi na akawashangaa watu wanaojipitisha katika jimbo hilo kwa kutumia lugha za uongo.

“Wanajua muda haujafika, wanavunja kanuni na wanapaswa kuchukuliwa hatua kwasababu wao ni wana CCM na wanapita katika majimbo yanayoongozwa na wana CCM wenzao,” alisema bila kuwataja watu hao.

Friday, 11 April 2014

TFDA YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA VIPODOZI ZAIDI YA 200

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imepiga marufuku vipodozi 222, baada ya kugundulika kuwa vina viambata vyenye sumu.
Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, alibainisha hayo alipozungumza na Tanzania Daima kwenye ofisi za mamlaka hiyo zilizopo eneo la Uzunguni jijini hapa.
Analanga alisema kuwa vipodozi hivyo vimepigwa marufuku baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa kimaabara ambapo uchunguzi huo umegundua kuwepo kwa viambata 11 vyenye sumu vinavyoweza kusababisha madhara kwa binadamu.
“Mpaka sasa tuna viambata 11 vya kisayansi ambavyo tumevichunguza na kugundua kuwa vina madhara kwa mtumiaji. Tumegundua karibu vipodozi 222  nchini vina viambata hivyo,’’ alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo TFDA inadhibiti uingizwaji na usambazaji wa vipodozi hususan kwenye mipaka rasmi kwa kuweka mawakala wa mamlaka hiyo kwa ajili ya kupima vipodozi vinavyoingizwa kwenye mipaka hiyo.
Alisema kuwa moja ya vipodozi vyenye sumu ambavyo ni changamoto kuvidhibiti ni mafuta ya Carolite ambayo hutumiwa na watu wengi licha ya kuwa na madhara ambayo ni ya muda mfupi na mrefu.
Aliyataja madhara ya muda mfupi yanayotokana na kipodozi hicho ni muwasho, kutokea kwa mabaka meusi ambapo madhara ya muda mrefu ni kansa ya ngozi ambayo hutokea baada ya sumu kujikusanya taratibu. 
Madhara mengine ni watoto kuzaliwa wakiwa na mtindio wa ubongo.
Analanga alitoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wanaouza na kuagiza vipodozi salama pamoja na kuonana na wataalamu wa TFDA ili kuhakiki vipodozi hivyo.

Thursday, 10 April 2014

ZIFAHAMU NCHI 20 ZENYE AMANI ZAIDI DUNIANI, KUTOKA AFRIKA IPO MOJA TU

1- DENMARK
Denmark

2-NORWAY
Norway

3-SINGAPORE
Singapore

4-SLOVENIA
Slovenia

5-SWEDEN
Sweden

6-ICELAND
Iceland

7-BELGIUM
Belgium

8-CZECH REPUBLIC
Czech Republic

9-SWITZERLAND
Switzerland

10-JAPAN
Japan

11-IRELAND
Ireland

12-FINLAND
Finland

13-NEW ZEALAND
New Zealand

14-CANADA
Canada

15-AUSTRIA
Austria

16-BHUTAN
Bhutan

17-AUSTRALIA
Australia

18-PORTUGAL
Portugal

19-QATAR
Qatar

20-MAURITIUS
Mauritius